Imewekwa: 03 Oct, 2026
DKT. KAVURA: URITHI WA ELIMU NA UONGOZI ULIOJENGA TPSC NA KULITUMIKIA TAIFA

DKT. KAVURA: URITHI WA ELIMU NA UONGOZI ULIOJENGA TPSC NA KULITUMIKIA TAIFA

Na Shakiru Abdulkarim

Uhai wa mwanadamu una mwisho, lakini mchango wake katika maisha ya wengine unaweza kuendelea kuishi kwa vizazi. Kifo cha Dkt. Richard Mwenyewe Kavura, kilichotokea tarehe 2 Oktoba 2026 nyumbani kwake Goigi, Mbezi Beach, Dar es Salaam, kimeacha pengo katika jumuiya ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), huku kikitukumbusha thamani ya urithi aliouacha. Akiwa Mkuu wa kwanza wa Chuo kuanzia mwaka 2000 hadi 2005, alikiongoza katika miaka yake ya mwanzo na kushiriki kuweka misingi ya mafunzo, tafiti na ushauri wa kitaalamu kwa ajili ya kuendeleza utumishi wa umma.

“Tunamkumbuka Dkt. Kavura kwa kuweka misingi muhimu ya maendeleo ya Chuo chetu. Uongozi wake katika miaka ya mwanzo uliunganisha mafunzo na mahitaji ya utumishi wa umma, na mchango huo utaendelea kuwa sehemu ya historia ya TPSC.” — Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu, Dkt. Ernest Mabonesho.

Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kimetimiza miaka 25 tangu kuanzishwa kwake. Katika sherehe za kilele cha Maadhimisho ya Miaka 25 ya Chuo, zilizofanyika tarehe 3 Julai 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, TPSC ilitambua mchango wa Dkt. Kavura na kumtunuku tuzo kwa mchango wake katika maendeleo ya Chuo.

KUTOKA MAKTABA: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mh. Ridhiwani Jakaya Kikwete, akimkabidhi Dkt. Richard Mwenyewe Kavura tuzo ya kutambua mchango wake katika maendeleo ya TPSC, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Miaka 25 ya Chuo, tarehe 3 Julai 2026, jijini Dar es Salaam.

Dkt. Kavura alizaliwa tarehe 22 Agosti 1944. Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Kakonko, wilayani Kibondo, na baadaye akasoma katika Shule ya Sekondari St. Mary’s, Tabora, na Shule ya Sekondari Shinyanga. Mwaka 1970, alihitimu Shahada ya Sanaa yenye Elimu katika eneo la Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, Dar es Salaam. Alipata Shahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Windsor, Canada, mwaka 1975, na Shahada ya Uzamivu katika Usimamizi kutoka Chuo Kikuu cha Cranfield, Uingereza, mwaka 1983.

Safari yake ya kulitumikia taifa kupitia elimu ilianza mwaka 1970 akiwa mwalimu katika Shule ya Sekondari Lindi, ambako alifundisha hadi mwaka 1971. Baadaye, alifundisha katika Shule ya Sekondari Shinyanga kuanzia mwaka 1971 hadi 1972. Katika kipindi hicho, alifundisha masomo ya Kiingereza, Historia na Jiografia.

Kuanzia mwaka 1972 hadi 1988, alifanya kazi katika iliyokuwa Taasisi ya Maendeleo ya Uongozi (IDM), Mzumbe, akiwa mhadhiri na baadaye mhadhiri mwandamizi. Alifundisha masomo ya masoko, utafiti wa masoko na usimamizi wa mauzo, pamoja na kushiriki katika programu za kuwajengea uwezo viongozi wa ngazi za juu. Aidha, aliongoza Idara ya Mafunzo ya Biashara na kufanya tafiti na kazi za ushauri katika masoko, rasilimali watu, mahitaji ya mafunzo na usimamizi wa taasisi.

Utumishi wake katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) ulimpa nafasi nyingine ya kuchangia maendeleo ya elimu ya juu nchini. Alikuwa Naibu Mkuu wa Chuo kuanzia mwaka 1988 hadi 1991, na Mkuu wa Chuo kuanzia mwaka 1991 hadi 1995. Mafanikio katika kipindi cha uongozi wake IFM yalihusisha kuongezeka kwa udahili kutoka takribani wanafunzi 600 hadi zaidi ya 1,000 na kuongezeka kwa idadi ya wahadhiri kutoka takribani 30 hadi 50. Pia, sifa za kitaaluma za wahadhiri ziliendelezwa kupitia masomo ya uzamili na uzamivu. Alichangia kuanzishwa kwa programu mpya za kitaalamu, zikiwemo za teknolojia ya habari, pamoja na kuboresha miundombinu na vifaa vya kufundishia.

Kuanzia mwaka 1995 hadi 1998, kupitia Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Dkt. Kavura alikuwa Mshauri Mkuu wa Kiufundi katika Taasisi ya Utawala wa Umma ya Lesotho (LIPAM). Katika nafasi hiyo, alishiriki katika kuimarisha usimamizi wa taasisi, mitaala, uwezo wa wakufunzi, miundombinu na shughuli za tafiti na ushauri.

Mwaka 1999 hadi 2000, alirejea IFM akiwa Mkurugenzi wa Shule ya Mafunzo ya Uzamili na Kituo cha Utafiti. Alisimamia maendeleo ya mafunzo ya uzamili, tafiti, machapisho na ushauri wa kitaalamu, pamoja na viwango vya ubora katika shughuli za kitaaluma.

Uzoefu huo ulikuwa msingi muhimu wa kuiongoza TPSC. Alipokuwa Mkuu wa kwanza wa Chuo mwaka 2000, alisimamia shughuli za mafunzo, tafiti na ushauri wa kitaalamu, huku akiongoza maboresho yaliyolenga kukiwezesha Chuo kukidhi mahitaji ya watumishi wa umma.

Katika kipindi chake cha uongozi, majengo na maeneo ya kufundishia yalifanyiwa ukarabati na upanuzi. Madarasa na ofisi ziliongezewa samani, na Chuo kikapata vifaa vya kazi na kujifunzia, vikiwemo kompyuta, vitabu na vifaa vya mafunzo.

Mchango mwingine muhimu ulikuwa kuelekeza mitaala katika mahitaji ya Programu ya Mageuzi ya Utumishi wa Umma. Chuo kilianzisha mafunzo katika uongozi, usimamizi, utawala na usimamizi wa kumbukumbu.

Idadi ya waliojiunga na mafunzo iliongezeka kutoka 2,166 mwaka 2000/2001 hadi 5,195 mwaka 2004/2005. Mapato yatokanayo na shughuli kuu za Chuo nayo yaliongezeka kutoka shilingi milioni 753 hadi shilingi bilioni 2.1 katika miaka hiyo.

Mbali na uongozi wa taasisi, Dkt. Kavura alishiriki katika kuandaa na kutoa mafunzo, kutathmini mahitaji ya mafunzo na kuandaa mipango ya maendeleo ya watumishi. Maeneo aliyoyafanyia kazi yalijumuisha uongozi, utawala bora, mipango ya kimkakati, usimamizi wa utendaji na rasilimali watu. Wasifu wake unaeleza ushiriki wake katika programu za mafunzo kwa wakuu wa wilaya, watumishi wa sekretarieti za mikoa na watumishi wa Ikulu.

Baada ya kustaafu TPSC, aliendelea kulitumikia taifa kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Kuanzia mwaka 2006 hadi 2010, alikuwa mtaalamu wa kujenga uwezo wa watumishi kupitia Programu ya Mageuzi ya Utumishi wa Umma. Majukumu yake yalihusisha kuendeleza sera na mikakati ya kujenga uwezo katika wizara, idara na wakala za Serikali, kushiriki katika kuandaa sera ya mafunzo kwa utumishi wa umma, na kusaidia uandaaji wa mipango ya maendeleo ya rasilimali watu.

Katika miaka iliyofuata, aliendelea kutoa ushauri wa kitaalamu katika mipango ya kimkakati, tathmini za mafunzo, usimamizi wa rasilimali watu na maboresho ya mifumo ya kazi. Miongoni mwa taasisi zilizotajwa katika wasifu wake ni Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, Shirika la Posta Tanzania, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini, pamoja na taasisi mbalimbali za Zanzibar.

Aidha, alichangia uongozi wa elimu kupitia ushiriki katika bodi na mabaraza ya taasisi, zikiwemo Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, IDM Mzumbe, Chuo cha Elimu ya Biashara na Taasisi ya Uhasibu Arusha.

Urithi wake wa kitaaluma unaonekana pia katika maandiko kuhusu huduma kwa wateja, maadili, uadilifu na uwajibikaji wa watumishi wa umma, mipango ya kimkakati, usimamizi wa utendaji na maendeleo ya taaluma.

Kwa TPSC, kumuenzi Dkt. Kavura ni kutambua msingi aliouweka na kuendelea kuujenga kupitia mafunzo yenye ubora, tafiti zinazojibu mahitaji halisi na ushauri unaosaidia kuboresha utendaji wa taasisi.

Buriani, Dkt. Richard Mwenyewe Kavura. Mwenyezi Mungu ailaze roho yako mahali pema peponi. Amina.

Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo