Imewekwa: 07 Oct, 2026
UJENZI WA TPSC TANGA KUIMARISHA UTOAJI WA ELIMU, WAZIRI KIKWETE ATAKA UKAMILIKE KWA WAKATI

Serikali imesisitiza umuhimu wa kukamilisha kwa wakati mradi wa ujenzi katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Kampasi ya Tanga, ili kuimarisha utoaji wa elimu na kuwezesha miundombinu hiyo kuanza kutumika.

Msisitizo huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, alipokagua maendeleo ya mradi huo. Ujenzi utakapokamilika, Kampasi hiyo inatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,000.

Mhe. Kikwete amesema majengo hayo yana umuhimu mkubwa katika kufanikisha malengo ya Serikali ya kuimarisha utoaji wa elimu mkoani Tanga.

“Sisi ndani ya Serikali tunajua umuhimu wa jengo hili, sio pambo bali tunataka kuona majengo haya yanakuwa kitovu cha kutoa elimu katika Mkoa huu wa Tanga,” amesema.

Amepongeza uongozi wa TPSC kwa usimamizi mzuri wa mradi na kueleza kuwa ameridhishwa na hatua iliyofikiwa. Aidha, ameonesha matarajio yake ya kuona jengo linakamilika na kuanza kutumika ifikapo Mei 2027.

“Natamani kuona mwezi Mei 2027 jengo liwe limekamilika na kuanza kutumika ili pia tuweze kuendelea na ujenzi wa majengo mengine ndani ya Kampasi hii,” amesema Mhe. Kikwete.

Katika kuhakikisha matarajio hayo yanafikiwa, amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi na kutekeleza kazi kwa kuzingatia ubora na muda uliokubaliwa. Ameonya kuwa kushindwa kutimiza makubaliano kunaweza kusababisha hatua za kumbadilisha mkandarasi kuchukuliwa.

Akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa TPSC, Dkt. Ernest Mabonesho, amesema kukamilika kwa ujenzi huo kutaiwezesha Kampasi kuhudumia wanafunzi 2,000. Amemshukuru Waziri kwa ufuatiliaji wa mara kwa mara na kwa kuuhimiza uongozi wa Chuo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mhe. Gilbert Kalima, ameishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuwekeza katika miundombinu ya TPSC mkoani humo.

Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Bi. Prisca Lwangili, amemshukuru Mhe. Kikwete kwa uongozi wake na ufuatiliaji wa maendeleo ya mradi huo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Mhe. Rdhiwani Kikwete  (wa pili kutoka kushoto) akipata maelezo ya mradi wa ujenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC) ulipofikia wakati alipotembelea mradi huo uliopo Kata ya Maweni, Kange mkoani Tanga.

Mwonekano wa jengo la mradi wa ujenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC) Kampasi ya Tanga.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (wa kwanza kushoto), akisisitiza jambo wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Kampasi ya Tanga, iliyopo Kange, Kata ya Maweni, mkoani Tanga. Wa pili kutoka kushoto ni Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa TPSC, Dkt. Ernest Mabonesho.

Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo