Imewekwa: 14 Jun, 2026
WAZIRI RIDHIWANI KIKWETE AWAASA WAHITIMU KUCHANGIA MAENDELEO YA TANZANIA KATIKA DIRA 2050

Mtwara, Juni 13, 2026 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete (Mb.), amewataka wahitimu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kutumia maarifa na ujuzi walioupata chuoni kuleta maendeleo na kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa kwa miaka mingi ijayo.

Akizungumza wakati wa mahafali ya 43 ya Chuo TPSC Kampasi ya Mtwara, yaliyofanyika leo, Mhe. Kikwete amewapongeza wahitimu 1,929 waliomaliza katika ngazi za Astashahada, Stashahada, na Shahada ya Kwanza, kutokana na juhudi, nidhamu, na uvumilivu walionyesha. Amesema kuwa kuhitimu ni mwanzo wa safari mpya ya kuwatumikia wananchi na taifa kwa ujumla, na kuwahimiza kuwa mabalozi wazuri wa chuo kwa kuzingatia maadili, uwajibikaji, uzalendo, na ubunifu katika maeneo yao ya kazi na maisha ya kila siku.

“Taifa linahitaji wataalamu wenye uwezo wa kutatua changamoto, kuleta ubunifu, na kuongeza tija katika sekta za umma na binafsi. Maarifa mliyoyapata yanapaswa kuonekana katika matendo yenye manufaa kwa jamii na nchi kwa ujumla,” amesema Mhe. Kikwete.

Ameongeza kuwa, Tanzania inaelekea katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inahitaji wataalamu wenye maarifa na umahiri wa kutekeleza maeneo mbalimbali ya kimkakati. Ameeleza matumaini yake kuwa wahitimu hawa watakuwa sehemu ya nguvu kazi itakayochangia kufikia malengo ya dira hiyo.

Vilevile, Waziri Kikwete amekipongeza chuo kwa kuendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa mafunzo kupitia mifumo ya mtandaoni, hatua ambayo imerahisisha upatikanaji wa elimu kwa makundi mbalimbali ndani na nje ya nchi. Ameisistiza serikali kuendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza ufanisi, kupunguza gharama za utoaji huduma, na kupanua wigo wa huduma kwa wananchi.

Katika hotuba yake, Waziri Kikwete amesisitiza umuhimu wa tafiti zenye ubora kwa ajili ya kutoa suluhisho la changamoto za maendeleo na kusaidia kufanya maamuzi yanayotokana na ushahidi. Hivyo, ameiagiza Menejimenti ya chuo kuendelea kuimarisha shughuli za utafiti ili ziwe na mchango mkubwa zaidi katika maboresho ya sera, mifumo, na huduma za umma.

Amepongeza pia juhudi za chuo katika ushirikiano na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi, ikiwemo Kenya School of Government na National School of Government ya Afrika Kusini, kama njia ya kuboresha ubora wa mafunzo na kuongeza hadhi ya taasisi hiyo.

Zaidi ya hayo, amewataka waajiri wa umma kuhakikisha watumishi wapya wanapelekwa kwenye Mafunzo Elekezi ya Awali kwa mujibu wa taratibu za serikali, ili kuwajengea uelewa wa maadili, kanuni, na utamaduni wa utumishi wa umma.

Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Kikwete aliwataka wahitimu kutumia elimu waliyoipata kuleta mabadiliko chanya katika jamii, kuwa wachapakazi, wazalendo, na waadilifu. Pia, amewapongeza wahitimu, uongozi wa chuo, wahadhiri, watumishi, wazazi, na walezi kwa kufanikisha mahafali haya muhimu.

Naibu Katibu Mkuu, Utumishi, Bw. Xavier Mrope Daudi akitoa salamu  amesema kuwa, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ndiyo wenye dhamana ya usimamizi wa rasilimali za nchi. Ameagiza vyuo vya elimu kuhakikisha wanaanda wahitimu vizuri ili kukidhi mahitaji ya soko na mazingira yanayowazunguka.

Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo Dkt. Ernest Mabonesho akiyoa taarifa ya utendaji wa chuo, amesema kuwa, katika mahafali haya, jumla ya wahitimu 1,929 watatunukiwa vyeti vya Astashahada, Stashahada, na Shahada katika fani mbalimbali. Kati yao, wahitimu 1,412 sawa na asilimia 73 ni wanawake, na wahitimu 517 sawa na asilimia 27 ni wanaume.

Aidha, Dkt. Mabonesho amesisitiza kuwa mazingira ya utumishi wa umma yanahitaji huduma za haraka, rahisi, na zinazowajibu wananchi kwa wakati. Hii inahusisha matumizi ya teknolojia za kidijiti, akili bandia, na maamuzi yanayozingatia ushahidi wa kisayansi, ili kuleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za umma. Katika kukabiliana na hali hiyo, chuo kimeanza kuboresha mafunzo kwa kutumia mifumo ya kisasa ya teknolojia ili kuandaa wahitimu wenye ujuzi wa kukabiliana na changamoto za nyakati hizi za kisasa.

Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo