Serikali imekitaka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kuwa mfano wa kuigwa katika utoaji wa huduma bora na matumizi ya lugha zenye staha kwa wateja, ikizingatiwa kuwa chuo hicho ndicho jiko kuu linalopika watumishi wote wa umma nchini tangu wanapoingia kazini hadi wanapostaafu.
Rai hiyo imetolewa leo, Juni 11, 2026, mkoani Mtwara na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Mrope Daudi, wakati akifungua rasmi Baraza la Sita la Wafanyakazi wa chuo hicho. Bw. Daudi amesema kuwa lugha ya kumhudumia mteja ni nyenzo muhimu katika utoaji wa huduma bora na zenye tija serikalini.
"Katika utekelezaji wa majukumu yenu, hakikisheni kuwa mnatumia lugha nzuri na yenye staha kwa kuwasikiliza na kuwahudumia vizuri wateja wenu. Tunaamini kuwa nyie ndio jiko la kupika watumishi wa umma, tangu wanapoingia katika utumishi wa umma hadi wanapotoka. Hivyo, ni lazima muwe mfano wa kuigwa na watu wengine," amesisitiza Bw. Daudi.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa TPSC, Dkt. Ernest Mabonesho, amesema kuwa chuo kimejipanga kikamilifu kuishi kulingana na matarajio hayo ya serikali. Amebainisha kuwa, kupitia baraza lenye wajumbe 64 kutoka kampasi zote sita, watapitia na kujadili Mpango Mkakati mpya wa Miaka Mitano (2026/27 – 2030/31) na bajeti ya mwaka ujao wa fedha ili kuboresha utendaji wao.
"Baraza hili ni chombo muhimu cha ushauri na majadiliano mahala pa kazi. Tunatambua kuwa Baraza ni chombo kinachowezesha ushirikiano, mawasiliano na mashauriano kati ya uongozi na wafanyakazi kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi, ustawi wa watumishi pamoja na maendeleo ya Taasisi yetu," alisema Dkt. Mabonesho.
Kikao cha 41 cha Utumishi wa Umma kinafanyika Mtwara kwa siku mbili kuanzia leo tarehe June 2026. Katika kikao hicho, Kikao kitajadili na kupitisha Mpango Mkakati mpya wa Miaka Mitano (2026/27 – 2030/31) ambao umebeba vipaumbele vikubwa vya kidijitali na uboreshaji wa mifumo ya utendaji kazi.

