Imewekwa: 04 Jul, 2026
TPSC YATAJWA KUWA KITOVU CHA MAGEUZI YA UTUMISHI WA UMMA NCHINI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Jakaya Kikwete, amesema Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kinaendelea kujijenga kuwa kitovu cha maendeleo ya rasilimali watu, tafiti tumizi na ushauri wa kitaalamu kitakachoiwezesha Tanzania kuwa na utumishi wa umma wenye ushindani katika Afrika Mashariki na Bara la Afrika.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya miaka 25 ya TPSC yaliyofanyika katika Julius Nyerere International Convention Centre, Kikwete amesema mafanikio yaliyopatikana ndani ya robo karne yanaonesha kuwa Chuo kimebadilika kutoka taasisi ndogo ya mafunzo na kuwa nguzo muhimu ya Serikali katika kuandaa watumishi wa umma wenye maarifa, stadi, maadili na uzalendo.

"Nina hakika kuwa kwa mipango iliyoelezwa katika taarifa ya Mkuu wa Chuo, pamoja na ushirikiano wa Serikali na wadau mbalimbali, Chuo kitaendelea kukua na kuwa moja ya taasisi bora zaidi za mafunzo ya utumishi wa umma katika ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla," alisema Kikwete.

Amesema kuwa, katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, TPSC kimepanua wigo wa huduma zake kutoka kampasi mbili hadi sita, huku kikianzisha mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu, mafunzo kwa njia ya mtandao, tafiti tumizi na huduma za ushauri wa kitaalamu zinazochangia kuimarisha utendaji wa Serikali.

Kikwete pia ameeleza kufurahishwa na hatua ya Chuo kuwekeza katika teknolojia za kisasa, ikiwemo Akili Mnemba (Artificial Intelligence), pamoja na kuimarisha tafiti tumizi kupitia uzinduzi wa tafiti sita zinazolenga kutoa suluhisho kwa changamoto za taasisi za umma.

Aidha, Kikwete amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan itaendelea kukiunga mkono chuo cha Utumishi wa Umma  ili kiweze kutekeleza wajibu wake wa kuandaa watumishi wa umma wenye uwezo wa kuhimili mabadiliko ya teknolojia na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akihitimisha hotuba yake, Kikwete aliwapongeza viongozi, wafanyakazi, wanafunzi, wahitimu na wadau wote wa TPSC kwa mchango wao katika mafanikio ya miaka 25 ya Chuo, akieleza imani yake kuwa miaka ijayo itakuwa ya mafanikio makubwa zaidi na kukifanya TPSC kuwa taasisi ya mfano katika maendeleo ya utumishi wa umma barani Afrika.

Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo