Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kimetoa mafunzo ya kuimarisha ujuzi na stadi za uongozi kwa viongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), yakilenga kuwajengea uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya kiutendaji, kuzingatia sheria na kanuni za utumishi wa umma, pamoja na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na uwajibikaji.
Mafunzo hayo ya siku tano yamefunguliwa tarehe 23 Novemba 2026 katika Kituo cha Mafunzo cha APC, Bunju, Dar es Salaam. Dar es Salaam, na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 27 Novemba 2026.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara wa TANAPA, Bw. Izumbe Msindai, aliyemwakilisha Waziri wa Maliasili na Utalii, aliipongeza TPSC na TANAPA kwa kuandaa mafunzo hayo. Alisema kuwa mafunzo hayo ni zaidi ya fursa ya kuongeza maarifa, kwani yanatoa nafasi kwa viongozi kujitathmini, kuimarisha utendaji wao na kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa ushirikiano, kwa kuzingatia sheria, maadili na miongozo ya kiutumishi.
“Tunapaswa kutambua kuwa TANAPA ni taasisi moja yenye dhamana kubwa kwa taifa. Mafanikio ya taasisi hii yanategemea menejimenti inayofanya kazi kwa mshikamano, inayoshirikishana katika maamuzi na inayowajibika kwa pamoja katika kutekeleza majukumu yake,” amesema Msindai.
Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Tafiti na Shauri za Kitaalam wa TPSC, Dkt. Hamisi Amani, aliyemwakilisha Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu, Dkt. Ernest Francis Mabonesho, amesema kuwa uongozi bora haupimwi kwa cheo au mamlaka aliyonayo mtu, bali kwa uwezo wake wa kutoa mwelekeo, kusimamia rasilimali na kuhakikisha taasisi inafikia malengo yaliyokusudiwa.
“Uongozi hauishii katika cheo, mamlaka au nafasi aliyonayo mtu. Uongozi bora hupimwa kwa uwezo wa kiongozi kutoa mwelekeo, kusimamia rasilimali kwa uadilifu, kuwajenga wengine na kuleta matokeo yanayoonekana katika taasisi,” alisema Dkt. Amani.
Ameeleza kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kwa kuzingatia wajibu mkubwa wa TANAPA katika kusimamia na kuhifadhi hifadhi za taifa, ambazo ni urithi wa taifa, vivutio muhimu vya utalii na chanzo cha mapato na maendeleo ya nchi. Hivyo, viongozi wanapaswa kuwa na maarifa, ujuzi na weledi unaowawezesha kutekeleza dhamana hiyo kwa ufanisi.
Aidha, Dkt. Amani amewahimiza washiriki kutumia fursa hiyo kushiriki kikamilifu katika mijadala, kuuliza maswali na kubadilishana uzoefu ili kuunganisha maarifa watakayopata na changamoto halisi za kiutendaji wanazokabiliana nazo katika maeneo yao ya kazi.
Amesisitiza kuwa TPSC itaendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na TANAPA katika kutoa mafunzo, kufanya tafiti tumizi na kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu kwa lengo la kuimarisha uwezo wa rasilimali watu na kuboresha utendaji wa taasisi za umma.

