02 May, 2026 09:00 AM-1:00 PM Mwalimu Julius Nyerere International Convention Centre

.

Kongamano la Pili la Kitaaluma la Utumishi wa Umma Tanzania 2026 ni jukwaa la kitaifa na kikanda litakalojadili nafasi ya utumishi wa umma katika kutimiza malengo ya Dira 2050 kwa Tanzania Bara na Zanzibar. Tukio hili lenye dhima ya “Nafasi ya Utumishi wa Umma wa Kisasa katika kufanikisha Malengo ya DIRA za Taifa 2050 ”, linatarajiwa kufanyika tarehe 18 Juni 2026 katika Ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), Dar es Salaam, chini ya uratibu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) na Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar (IPA). Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (Ufunguzi), au Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt Hussen Ali Mwinyi kama ambavyo Waziri wa Utumishi Tanzania bara ataona inafaa.

Washiriki wa kongamano wanatarajiwa kuwa viongozi wa serikali na watunga sera, wataalamu wa utumishi wa umma (rasilimali watu na TEHAMA), wataaluma, sekta binafsi hususan katika tasinia ya teknolojia na kifedha, mashirika ya kiraia, wadau wa maendeleo na utumishi wa umma wa kikanda na kimataifa, pamoja na viongozi chipukizi na wanafunzi wa masuala ya utawala. Wanahabari na wataalamu wa mawasiliano pia watahusika ili kuhakikisha matokeo ya kongamano yanawafikia wananchi kwa upana.

 

Kongamano linalenga kupanua upeo wa mijadala kuhusu mageuzi ya taasisi za umma, uwajibikaji, ufanisi wa kiutawala, na nafasi ya teknolojia na ubunifu katika kuboresha huduma kwa wananchi. Wakati Dira ya Taifa Tanzania Bara 2050 inalenga kujenga uchumi wa viwanda na maarifa, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 inajikita katika uchumi wa buluu, utalii, kilimo cha thamani ya juu na sekta za kidijitali. Ingawa njia za ukuaji zitakuwa tofauti, zote zinashabihiana katika lengo la kujenga jamii yenye kipato cha kati cha juu na utumishi wa umma wenye ufanisi na uwajibikaji.

Kwa jumla, kongamano hili linatarajiwa kuwa chachu ya kuunganisha wadau wote muhimu katika safari ya kuelekea Tanzania ya kisasa yenye utumishi wa umma bunifu na wa mabadiliko ifikapo mwaka 2050.

KONGAMANO LA PILI LA KITAALUMA LA UTUMISHI WA UMMA TANZANIA
Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo