Imewekwa: 29 Mar, 2026
CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA KAMPASI YA SINGIDA CHATOA MSAADA KWA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM

Machi 28, 2026 — Ititi, Singida

Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 25 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Kampasi ya Singida imetoa msaada kwa watoto wenye mahitaji maalum wanaolelewa katika kituo cha Malaika wa Matumaini kilichopo Ititi, mkoani Singida.

Zoezi hilo limeongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhe. Godwin Gondwe, akiambatana na Mkurugenzi wa Kampasi ya Singida, Dkt. Emmanuel Tandika, pamoja na watumishi wa chuo hicho. Timu hiyo ilikabidhi msaada uliokuwa na vyakula mbalimbali kama mchele, sukari, unga wa sembe na vifaa vya usafi, sambamba na kushiriki shughuli za usafi katika eneo la kituo hicho.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Gondwe, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, amekipongeza Chuo cha Utumishi wa Umma kwa moyo wa kujitolea na kuguswa na jamii, akisema kitendo hicho ni mfano wa kuigwa na taasisi nyingine.

“Kitendo hiki kinaunga mkono juhudi za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye amekuwa akiwajali wenye uhitaji, hususan watoto katika nyanja za elimu na afya,” alisema Mhe. Gondwe.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampasi ya Singida, Dkt. Emmanuel Tandika, amesema kuwa msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa dhima ya chuo katika kuchangia maendeleo ya jamii.

“Tunaposherehekea jubilee ya miaka 25 ya kuutumikia umma wa Watanzania, Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida kimeona ni vyema kutoa mchango wake kwa watoto hawa wenye mahitaji maalum kwa kuwaonyesha moyo wa upendo na kuwaonesha kwamba jamii inawajali,” alisema Dkt. Tandika.

Ameongeza kuwa msaada huo pia unalenga kuwapa motisha masista na walezi wanaowalea watoto hao licha ya changamoto nyingi wanazokabiliana nazo.

Naye Mlezi wa Kituo cha Malaika, Sista Rosalia Nicodemus, kwa niaba ya Mkuu wa Shirika, aliwashukuru uongozi wa Chuo cha Utumishi wa Umma pamoja na serikali ya mkoa kwa msaada huo, akisema umeleta faraja na matumaini kwa watoto wanaolelewa kituoni hapo.

“Watoto hawa mara nyingi hukumbwa na changamoto ya upweke, hivyo wanapopata wageni wanaowatembelea, hufurahia na kujiona kuwa ni sehemu ya jamii,” alisema Sista Rosalia.

Aidha, alitoa shukrani kwa wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakitembelea kituo hicho na kuuomba mashirika na taasisi nyingine kuendelea kuunga mkono juhudi hizo kupitia misaada na upendo kwa watoto hao.

Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania katika kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, kimekuwa kikifanya shughuli mbalimbali za kijamii kupitia kampasi zake za Dar es Salaam, Tabora, Tanga, Singida, Mtwara na Mbeya, kuelekea kilele cha maadhimisho hayo yatakayofanyika mwezi Juni 2026

 

Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo