Imewekwa: 27 Nov, 2025
CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA NI MUHIMU KATIKA KUBORESHA UTUMISHI WA UMMA NCHINI-KIKWETE

CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA NI MUHIMU KATIKA KUBORESHA UTUMISHI WA UMMA NCHINI-KIKWETE

Dar es Salaam,  Novemba 28, 2025

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete amesema kuwa Chuo cha Utumishi wa Umma ni kiungo muhimu katika kuboresha sekta ya utumishi wa umma nchini.

Kauli hiyo ameitoa wakati akiongea na Menejimenti ya Chuo cha Utumishi Umma Tanzania katika ziara yake ya kikazi aliyoifanya leo katika makao makuu ya chuo yaliyopo barabara ya Bibi Titi Mohamed, Dar es Salaam. Mhe. Kikwete amesisitiza kuwa, katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Chuo kina jukumu la kutoa mwelekeo wa Utumishi wa umma kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.

“Nchi yetu sasa inaingia katika Utekelezaji wa Dira ya 2050, lazima kama chuo cha Utumishi wa Umma tujiulize utumishi wa Umma unakwenda wapi itakapofika mwaka 2050” ameongeza Mhe. Kikwete.

Katika utekelezaji wake Mhe. Ridhwani amesisitiza chuo kuendelea kufanya tafiti tumizi zitakazoweza kuboresha mahitaji ya mafunzo kwa watumishi wa umma, changamoto zinazokabili Utumishi wa Umma nchini na mapendekezo ya utatuzi wake ili kuishauri serikali jinsi ya kuboresha Utumishi wa Umma nchini.

Pia , Mhe. Kikwete amekipongeza Chuo cha Utunmishi wa Umma kwa hatua za maendeleo na kuahidi wizara kuendelea kukisaidia chuo katika kutekeleza majukumu yake ili kiweze kutoa mchango wako wa kuboresha utumishi wa umma nchini.

Naye Bw. Nolasco Kipanda, Mkurugenzi wa Uendelezaji Taasisi aliye mwakilisha Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, amekipongeza Chuo cha Utumishi wa Umma kwa utendaji kazi wake katika nyanja zote za mafunzo kwa watumishi wa umma, taaluma, tafiti, na shauri za kitaalamu.

"Najivunia maendeleo ya Wakala hii ya Serikali katika kutoa huduma ya mafunzo kwa ufanisi, weledi na ubora tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000," amesema Bw. Kipanda.

Aidha, amesisitiza kuwa, anawasihi watumishi wa chuo hicho kuendelea kuchapa kazi kwa weledi ili kufanikisha malengo ya kuanzishwa kwake na kufanikisha maono ya Mheshimiwa Rais kuhusu uboreshaji wa utumishi wa umma

Akitoa taarifa ya Utendaji katika kipindi cha miaka minne (2021/22 – 2024/25), Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania , Dkt. Ernest Mabonesho amesema kuwa Chuo kimefanikiwa kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma 46,964 sawa na wastani wa watumishi 11,741 kwa mwaka.

Dkt. Mabonesho ameongeza kuwa, kwa upande wa mafunzo ya muda mrefu, Chuo kimefanikiwa kudahili na kuendesha mafunzo kwa jumla ya wanachuo wapatao 43,753 katika ngazi ya Shahada, Stashahada na Astashahada, katika Menejimeti ya Kumbukumbu, Nyaraka, naTaarifa; Uhazili na Utawala; Utawala wa Umma; Menejimenti ya Rasilimali watu; na Ununuzi & Ugavi. Pia, amesema kwa, Chuo kimefanikiwa kutoa jumla ya shauri 27 kwa taasisi kadhaa za umma nchini na kukamilisha a jumla ya tafiti tumizi nane (08) kuhusu masuala mtambuka katika Utumishi wa umma.

Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo