Imewekwa: 13 Feb, 2026
SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI SAHIHI YA TEKNOLOJIA ZA KISASA KUIMARISHA UTENDAJI SERIKALINI

Dar es Salaam, 12 Februari 2026

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi, amesisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia za kisasa, ikiwemo Akili mnemba (AI), katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa ufanisi zaidi, uwazi na uwajibikaji wa watumishi wa umma nchini. Ameyasema hayo wakati akifungua rasmi Mdahalo wa Kitaalamu kuhusu Matumizi ya Akili Mnemba, ulioandaliwa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania katika Kituo cha Mafunzo kwa Njia ya Mtandao jijini Dar es Salaam.

Bw. Daudi amesema, serikali inaendelea kuhimiza matumizi sahihi ya teknolojia za kisasa kama sehemu ya mkakati wa kisera wa kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya rasilimali fedha na kuongeza uwazi katika taasisi za serikali. Pia, amekipongeza Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kwa kuandaa mdahalo huo unaotoa jukwaa kwa watumishi wa umma, wataalamu wa teknolojia na wadau wengine kubadilishana uzoefu kuhusu matumizi ya Akili mnemba katika kuongeza tija na ufanisi wa kiutumishi.

Aidha, Bw. Daudi amesisitiza kuwa teknolojia za kisasa zinapaswa kutumika kwa kuzingatia maadili, mipaka na changamoto zinazoweza kutokea wakati wa utekelezaji wake. Ameeleza  kuwa Akili Mnemba inapaswa kuwa nyenzo ya kumsaidia mtumishi wa umma kuongeza ufanisi wa kazi, si kuchukua nafasi ya binadamu.

“Akili mnemba haichukui nafasi ya mtumishi wa umma, bali ni chombo cha kumsaidia kutoa huduma bora, kwa wakati na kwa ufanisi zaidi,” amesema Bw. Daud.

Awali, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa TPSC, Dkt. Ernest Mabonesho akitoa neno la utangulizi amesema Kuwa, chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kimejipanga kuhakikisha kinaendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza ubora wa utumishi wa umma kupitia mafunzo, mijadala ya kitaalamu na tafiti za teknolojia.

Mdahalo huo ulihusisha watunga sera, wataalamu wa teknolojia, wanasayansi wa data, wasomi, pamoja na wawakilishi kutoka wizara, taasisi, idara na wakala mbalimbali wa serikali. Washiriki walijumuika ana kwa ana na wengine walishiriki kwa njia ya mtandao, hatua iliyowezesha mjadala huo kuwa wa kina, shirikishi na wenye tija katika kuimarisha matumizi ya teknolojia ya Akili mnemba ndani ya utumishi wa umma nchini

Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo