Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Tanga, leo tarehe 20 Februari 2026. Hafla hiyo imefanyika katika eneo la mradi mtaa wa Kange Uzunguni, jijini Tanga.
Akiongea baada ya kuweka jiwe la msingi, Mhe Kikwete amesema, serikali itatenga jumla ya shilingi bilioni 39 kwa ajili ya ujenzi wa kampasi hiyo, fedha zinazotarajiwa kutengwa kila mwaka hadi kukamilika kwa mradi huo. Amemshukuru Mhe. Rais kwa kuruhusi kiasi hicho kutengwa kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi hiyo.
“Namshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuruhusu kutengwa kwa kiasi cha shilingi bilioni 39 kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi ya Tanga.”
Aidha, Mhe. Kikwete amesema kuwa, mradi huu lujengwa tena ni jitihada za serikali kuinua Uchumi wa mkoa wa Tanga na utakapomalizika utaleta manufaa makubwa kwa wananchi kiuchumi, ikiwemo kuimarisha ajira na maendeleo ya kijamii, na kuonyesha dhamira ya serikali kuimarisha sekta ya elimu na utumishi wa umma nchini.
Pia Mhe Kikwete baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo kabala ya kuweka jiwe la msingi amesema kuwa, ameridhishwa na kiwango cha ujenzi unaendelea. Ameipongea menejeimenti ya chuo cha Utumishi wa Umma kwa usimamizi mzuri katika ujenzi wa Kampasi.
Kwa upande wa Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Ernest Mabonesho akitoa taarifa ya mradi amesema kuwa, mradi wa ujenzi wa Kampasi ya Tanga awamu ya kwanza ya ujenzi wa jengo la Taaluma ulianza rasmi tarehe 8 Februari 2025.
Amesema kuwa jengo hilo lenye ghorofa mbili litakuwa na madarasa 26, yatakayohudumia zaidi ya wanafunzi 2,500 kwa wakati mmoja. Pia Jengo hilo litakuwa na ofisi 24 za watumishi, kumbi mbili za mikutano, na vyoo vya kisasa 18, sambamba na miundombinu ya kisasa ya TEHAMA itakayowezesha matumizi bora ya teknolojia katika kufundisha na kufanya kazi za kitaaluma.
Kampasi ya Tanga ni miongoni mwa kampasi sita za chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania iliyoanzishwa rasmi Januari 2013 katika majengo ya kukodi ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi. Ujenzi wa mradi kuu unakiwezesha chuo kuboresha miundo mbinu ili kutoa huduma bora zaidi.




