Imewekwa: 29 Nov, 2025
WAZIRI KIKWETE AKITAKA CHUO KUENDELEA KUFANYA TAFITI ZITAKAZOSAIDIA KUBORESHA UTUMISHI WA UMMA NCHINI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amekitaka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kuendelea kufanya Tafiti zinazolenga kutatua changoto za muda mrefu kwenye Utumishi wa Umma hivyo kuleta tija katika kutekeleza mpango wa dira ya maendeleo 2050.

Mhe. Kikwete ameyasema hayo wakati wa Mahafali ya 42 ya Chuo cha Utumishi wa Umma yaliyofanyika tarehe 28 Novemba, 2025 katika Ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini, Dar es salaam.

Pia, Mhe. Kikwete ameielekeza Menejimenti ya Chuo cha Utumishi Umma Tanzania kujipambanua vizuri katika kutoa mafunzo ya muda mrefu ili malengo yaliyokusudiwa kwenye dira ya maendeleo ya 2050 yaweze kufikiwa kikamilifu. Waziri Kikwete amesisitiza umuhimu wa kujifunza maisha yote na kuendelea kujifunza baada ya kuhitimu, ili kukidhi mahitaji yanayobadilika kila wakati. Alieleza kuwa wahitimu wanapaswa kuwa mabalozi wa maadili, uzalendo, na weledi katika sekta mbalimbali za umma na binafsi.

Aidha Mhe waziri Kikwete ameipongeza Bodi, Menejimenti na Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma akisema mahafali haya yanafanyika katika mwaka wa kihistoria ambapo Chuo cha Utumishi wa umma Tanzania kimetimiza miaka 25 tangu kuanzishwa kwake. Hii ni robo karne ya kujenga uwezo, kukuza weledi, kuimarisha maadili ya utumishi wa umma na kutekeleza majukumu ya msingi katika kusimamia rasilimaliwatu serikalini.

Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu-UTUMISHI, Bw. Nolasco Kipanda amesema kuwa  katika kipindi cha miaka 25, Chuo kimepiga hatua kubwa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa kampasi kutoka mbili hadi sita na hivyo kusogeza huduma karibu na watumishi, kuongeza wigo wa kozi za muda mrefu hadi kufikia ngazi ya shahada ya kwanza, kuimarisha mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi wa umma, kuongeza wigo wa matumizi ya tehama katika mafunzo, kuboresha miundombinu kwa kukamilisha ujenzi wa kampasi ya singida na kuanza ujenzi wa kampasi ya tanga, pamoja na kuimarisha shughuli za tafiti, machapisho na ushauri wa kitaalamu unaochochea maboresho ya sekta ya umma.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Frolens Turuka akitoa salamu za Bodi, amewashukuru wahitimu wote waliomaliza salama na kutunukiwa vyeti, huku akiwataka wahitimu kutumia maarifa waliyoyapata kwa manufaa yao binafsi na taifa kwa ujumla.

Dkt. Turuka amesema kuwa wao kama Bodi wataendelea kushauri ipasavyo ili kuimarisha uwezo wa Sekta ya Umma, kwa kuendana na mabadiliko ya teknolojia, na kuhakikisha kuwa yale yote yanayopaswa kufanyika katika utumishi wa umma yanatekelezwa kwa ufanisi.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Mkuu wa Chuo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo Dkt. Ernest Mabonesho amesema chuo kimeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kutoa mafunzo, kufanya tafiti, kutoa ushauri wa kitaalamu na kusimamia miradi ya maendeleo.

Aidha, Dkt. Mabonesho amesema kuwa jumla ya wanachuo 6,956, wamehitimu masomo yao na wanatunuku vyeti kulingana na taaluma na fani zao. Pia katika mafunzo ya muda mfupi ya kuwajengea uwezo watumishi wa Umma, katika mwaka huu wa fedha wa 2024/2025, Chuo kimewafikia jumla ya watumishi 12,189, Kufanya Tafiti na Shauri za Kitaalamu na kukamilisha jumla ya tafiti tumizi nane (08) kuhusu masuala mtambuka katika Utumishi wa Umma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete, akiongoza Maandamano ya Kitaaluma katika Mahafali ya 42 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) tarehe 28.11.2025 leo jijini Dar es Salaam

 

Sehemu ya Wahitimu wa Mahafali ya 42 ya Chuo cha Utumishi wa umma Tanzania (TPSC) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa mahafali hayo yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) tarehe 28.11.2025 leo jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, akimkabidhi zawadi mwanafunzi hodari, Luka Bita, aliyehitimu Shahada ya Kwanza katika fani ya Utunzaji wa Kumbukumbu, Nyaraka na Taarifa, katika mahafali ya 42 ya Chuo cha Utumishi wa Umma yaliyofanyika tarehe tarehe 28.11.2025 leo jijini Dar es Salaam

 

 

 

Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo