Imewekwa: 22 Oct, 2025
KATIBU MKUU MKOMI ARIDHISHWA NA KASI NA VIWANGO VYA UJENZI WA KAMPASI YA TANGA

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Selemani Mkomi, amesema hayo tarehe 20 Oktoba 2025, alipotembelea mradi wa ujenzi wa jengo la Kampasi ya Tanga, unaotekelezwa eneo la Kange, Jijini Tanga, katika kiwanja chenye ukubwa wa hekta 5.7. 

Akiongea baada ya kutembelea mradi na kupokea taarifa za utekelezaji wa mradi huo, Katibu Mkomi amesema ameridhishwa na viwango na maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo. Ameelekeza kuwa ni muhimu mradi kuzingatia viwango vya ubora na kukamilika kwa wakati uliopangwa, kulingana na mkataba, ili kuboresha miundombinu ya utoaji huduma kwa chuo.  Aidha, amesisitiza kuwa serikali itaendelea kutoa fedha ili kuhakikisha mradi unakamilika kama ilivyopangwa, kwa lengo la kuboresha utoaji huduma kwa wanafunzi na mazingira bora ya kazi kwa watumishi. 

Kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu, Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Dkt. Ernest Mabonesho, alitoa taarifa kuhusu maendeleo ya mradi huo. Alisema kuwa, awamu ya kwanza ya ujenzi wa Kampasi ya Tanga unahusisha jengo la taaluma litakalokuwa na madarasa 26, lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,500 kwa mkupuo mmoja, pamoja na ofisi 24 za watumishi.   Dkt. Mabonesho aliongeza kuwa,kukamilika kwa mradi wote utajumuisha jumla ya majengo 12, ikiwemo madarasa, ofisi za utawala, kumbi za mikutano, nyumba za wafanyakazi, mabweni ya wasichana na wavulana, maabara, maktaba, na jengo la mgahawa. 

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Watumishi Housing, Sephania Solomini, ambaye ni mtaalamu mshauri, amesema kuwa jengo litakuwa la kisasa, likikidhi mahitaji ya kisasa ya utoaji huduma kwa wanachuo kwa njia ya teknolojia. Amesema kuwa ujenzi wa jengo la ghorofa mbili uko katika hatua ya msingi, ambapo nguzo za sakafu ya chini (ground floor) na formworks za sakafu ya pili (first floor) zinaendelea kujengwa. Kukamilika kwa jengo hili kunakadiriwa kugharimu takribani shilingi bilioni 6.1.

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Selemani Mkomi (wa pili kutoka kushoto), akizungumza mara baada ya kufanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa jengo la Kampasi ya Tanga, katika ziara iliyofanyika tarehe 20 Oktoba jijini Tanga.

 

Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Dkt. Ernest Mabonesho (wa pili kutoka kulia), akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Selemani Mkomi (wa kwanza kutoka kulia) kuhusu mradi wa ujenzi wa Kampasi ya Tanga, wakati wa ziara ya Katibu Mkuu kutembelea mradi tarehe 20 Oktoba jijini Tanga.

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Selemani Mkomi (wa tatu kutoka kushoto), akipata maelezo kutoka kwa mkandarasi ( hayupo katika picha) wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa jengo la Kampasi ya Tanga, katika ziara iliyofanyika tarehe 20 Oktoba jijini Tanga.

Sehemu ya  Jengoo la Kampasi ya Tanga   litakalokuwa na madarasa 26, pamoja na ofisi 24

Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo