Imewekwa: 13 Dec, 2023
MHE.SIMBACHAWENE ASEMA UTUMISHI WA UMMA NI KUJITOA KUHUDUMIA WATU

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene ametoa rai kwa wahitimu kutambua kuwa kwenye utumishi wa umma sio sehemu ya kuvuna utajiri na kujilimbikizia mali bali ni sehemu ya kujitoa kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa umma.

Mhe. Simbachawene ametoa rai hiyo wakati wa mahafali ya 38 ya Chuo cha Utumishi wa umma Tanzania yaliyofanyika katika Kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Mkoani Tabora.

“Naomba kila mmoja wenu awe na moyo wa kujitoa kwa maendeleo ya taifa na kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana katika mazingira yenu na zile zinazotolewa na Serikali katika kujiletea maendeleo na kuhakikisha mnatatua changamoto zinazokabili jamii zinazowazunguka wakati mkidumisha amani, upendo na mshikamano” amesisitiza Mhe. Simbachawene.

Aidha, Mhe. Simbachawene ametumia fursa ya mahafali hayo kutoa wito kwa waajiri wote wa Taasisi za Umma nchini kukitumia Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania katika kuboresha utendaji kazi wa watumishi na Taasisi zao kupitia mafunzo mbalimbali yanayotolewa na Chuo hicho.

Mhe. Simbachawene amesema kuwa baadhi ya taasisi za umma zimekuwa zikisuasua katika kuwapatia waajiriwa wapya Mafunzo Elekezi ya Awali (Induction Training) jambo ambalo linasababisha watumishi hao kushindwa kutambua misingi ya Utumishi wa Umma, Sheria, Kanuni, Miongozo na Taratibu za utendaji kazi na uwajibikaji Serikalini.

Aidha, amewasisitiza Maafisa Masuuli wote katika taasisi za umma kutumia muda wao kufanya uchunguzi kwa makini ili kuona namna wajiriwa hao wapya wanavyopata shida katika utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi na hivyo kukwamisha jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Napenda ifahamimike kuwa suala la kuwapatia watumishi wapya mafunzo sio hiari bali ni matakwa ya kisheria na hii ni kwa mujibu wa waraka wa Utumishi Na. 5 wa mwaka 2011. Kwa hiyo ninaelekeza watumishi wote wapya katika utumishi wa umma wapewe mafunzo mara tu wanaporipoti katika vituo vyao vya kazi” amesisitiza Mhe. Simbachawene.

Vilevile, Mhe. Simbachawene ameipongeza Bodi, Menejimenti na watumishi wote wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa kuwa matunda ya kazi yao njema yanaonekana wazi. Vilevile amewahakikishia kuwa Serikali hii ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatambua juhudi wanazofanya na  hivyo, Wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano ili kufanikisha malengo ya chuo.

 

Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo