Dar es Salaam, 4 Machi 2026
Katika kuelekea Maadhimisho ya Miaka 25 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), wanawake wa chuo Dar es Salaam, wametembelea Gereza la Wanawake Segerea, jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo imeambatana na utoaji wa misaada kwa wafungwa na Mahabusu wanawake pamoja na watoto wanaoishi gerezani na wazazi wao, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Siku ya Wanawake Duniani.
Wakati wa ziara hiyo, walikabidhi mahitaji mbalimbali ikiwemo vyakula, sabuni, mafuta ya kujipaka, vitenge na kanga, mashuka, taulo za kike, maziwa ya watoto, nepi, vitabu vya dini, dawa za mswaki, miswaki pamoja na vifaa vya kufanyia usafi.
Akizungumza wakati wa kupokea misaada hiyo, Mkuu wa Gereza la Wanawake Segerea, SSP Amida Musa Matimba amewashukuru akina mama wa TPSC kwa kutenga muda wa kuwatembelea wanawake wafungwa na kuwafariji kupitia zawadi walizotoa. Amesema kuwa wanawake walioko gerezani bado ni sehemu ya jamii kama wanawake wengine, hivyo kusaidiwa kwao kunawapa faraja kubwa na kuwakumbusha kuwa hawajasahaulika.
SSP Matimba ameongeza kuwa Jeshi la Magereza linaendelea kutoa mafunzo mbalimbali ya ujuzi kwa wafungwa ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea mara watakapotoka gerezani. Aidha, amesema vitabu vya dini vilivyotolewa vitakuwa msaada mkubwa katika kuwaimarisha kiimani, hatua ambayo ni muhimu katika mchakato wa urekebu kwa wafungwa.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa chuo, Meneja wa Kituo cha Mafunzo kwa Njia ya Mtandao kutoka TPSC, Bi. Zena Hussein, amesema kuwa utoaji wa misaada hiyo umefanyika mahususi katika Wiki ya Wanawake Duniani na ni sehemu ya kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.
Amesisitiza kuwa chuo kitaendelea kushirikiana na jamii katika kutekeleza shughuli za kijamii zenye lengo la kuwatia moyo na kuwawezesha makundi maalum yenye uhitaji..
Hatua ya wanawake wa TPSC kutembelea gereza hilo ni katika imetajwa kuwa ni mchango muhimu kuimarisha mshikamano na kuunga mkono juhudi za kujenga jamii yenye usawa, huruma na mshikamano hasa kwa makundi yenye uhitaji maalum.

