Mbeya- Jumanne, Machi 31, 2026
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomon Itanda, ameongoza watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Kampasi ya Mbeya katika shughuli za kijamii za kutembelea vituo vya watoto yatima jijini Mbeya. Ziara hiyo iliwahusisha pia Mkurugenzi wa Kampasi ya Mbeya, Ndugu Saidy Nzagamba, ambapo walitembelea Kituo cha Watoto Yatima Iwambi kilichopo mtaa wa Iwambi na Kituo cha Bi Aisha Foundation kilichopo mtaa wa Soweto.
Katika ziara hiyo, TPSC Kampasi ya Mbeya imekabidhi mahitaji mbalimbali kwa ajili ya watoto hao, yakiwemo mchele, maharage, sabuni, juisi, mafuta ya kupikia, vitunguu, na mbuzi kwa ajili ya lishe na mahitaji ya kila siku.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Itunda, ameipongeza TPSC kwa maadhimisho yenye dhamira ya kugusa maisha ya watu. Alisema hatua hiyo inaonyesha utu na maadili ya utumishi wa umma yanayojengwa na chuo hicho.
"Chuo hiki kimeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa taifa letu kwa kutoa watumishi bora. Kila kinachofanywa hapa kinaonyesha dhamira ya kweli ya kuwahudumia wananchi na kujenga jamii yenye mshikamano," amesema Mhe. Itanda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampasi ya Mbeya, Ndugu Saidy Nzagamba, amesema kuwa chuo hicho kimeamua kushiriki na kusaidia watoto yatima kama sehemu ya kuwajengea faraja na kuwahakikishia kuwa jamii inawajali.
"Tunatambua changamoto wanazokabiliana nazo watoto hawa, ndiyo maana tumeamua kuwa jirani nao na kuwagusa kwa upendo. Huu ni mwanzo wa dhamira yetu kuendelea kushiriki shughuli za kijamii katika siku zijazo," amesema Nzagamba.
Viongozi wa vituo vya Iwambi na Bi Aisha Foundation wameushukuru uongozi wa TPSC Kampasi ya Mbeya kwa upendo na michango iliyotolewa, wakisema misaada hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa katika malezi na ustawi wa watoto.

