Mafunzo ya Wiki saba yanayohusu matumizi ya ujuzi wa kidigiti (Digital Skills) kwa Watumishi wa Mahakama 1,829 yamefunguliwa kwa pamoja leo tarehe 19/02/2024 katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma.
Mafunzo hayo yamefunguliwa na Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Victor Kategere kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania (JoT), ambapo kwa upande wa Dar es Salaam yanafanyika katika Kumbi za Kituo cha Mafunzo kwa Njia ya Mtandao cha Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) huku kwa Dodoma ni katika Ukumbi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
Mafunzo haya yanawezeshwa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania ( TPSC) - Kitengo cha Mafunzo kwa Njia ya Mtandao kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambao ni wasimamizi wa Mafunzo hayo.
Miongoni mwa malengo ya mafunzo haya ni kuwapatia na kukuza maarifa na ujuzi wa washiriki ili kuweza kutumia mifumo ya kidigiti katika kazi zao za Kimahakama, ikizingatiwa kuwa kwa sasa utendaji kazi wa Mahakama unaelekea zaidi mtandaoni (e-judiciary).
Aidha mafunzo haya yanafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kupitia mkopo wa Benki ya Dunia nani ni utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Maboresho ya Mahakama ya Tanzania.