
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Selemani Mkomi, amezindua rasmi Bodi mpya ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) katika hafla iliyofanyika leo tarehe 29 Septemba, 2025, jijini Dar es Salaam. Uzinduzi huo umefanyika katika Sehemu ya Mafunzo kwa njia ya Mtandao ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Bw. Mkomi alieleza kuwa uzinduzi wa Bodi ya Chuo cha Utumishi wa Umma ni hatua muhimu katika kuboresha utawala bora na ufanisi katika sekta ya utumishi wa umma nchini. Amesema, “Ukiboresha Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, umeboresha Utumishi wa Umma.”
Bw. Mkomi amewapongeza wajumbe wapya wa Bodi na kueleza kuwa uteuzi wa wajumbe wa bodi umezingatia sifa za weledi, uadilifu, na uzoefu wa kina katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuimarisha Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania. Alisisitiza kuwa majukumu makuu ya bodi ni kuhakikisha chuo kinatoa mafunzo yanayokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa, kutoa ushauri wa kitaalam, na kuchangia maendeleo ya sekta ya utumishi wa umma kwa ujumla.
Aidha, Bw. Mkomi amesisitiza kuwa bodi inapaswa kutoa dira na ushauri wa kimkakati utakaoleta mafanikio makubwa kwa chuo, kama kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundisha, matumizi bora ya rasilimali, na kuimarisha nidhamu kazini. Aliongeza kuwa kuboresha Chuo cha Utumishi wa Umma ni hatua muhimu ya kuimarisha utumishi wa umma nchini, na serikali itaendelea kutoa miongozo na sera zitakazosaidia maendeleo ya chuo na sekta kwa ujumla.
Halikadhalika, Bw. Mkomi ametambua mchango wa bodi iliyopita na kuwatakia kila la heri wajumbe wa bodi mpya walioteuliwa. Amewaomba waendelee kuonyesha maadili na weledi wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yao, huku akiahidi kuwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora iko tayari kushirikiana nao kikamilifu katika kutekeleza majukumu yao.
Akitoa taarifa ya Utendaji ya Bodi iliyomaliza muda wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Florens Turuka, amesema kuwa, katika kipindi cha miaka minne, bodi ilifanikiwa kuimarisha utendaji wa chuo, ikiwemo kupatikana kwa hati safi za ukaguzi wa hesabu za serikali kwa miaka minne mfululizo, jambo ambalo ni alama ya uwajibikaji wa kiutendaji na usimamizi wa fedha unaoongozwa na uwazi.
Ameongeza kuwa bodi iliweza kuidhinisha sera na mifumo mbalimbali ya kitaasisi, ikiwemo sera za utafiti, teknolojia ya habari, usimamizi wa hatari, ubora wa huduma na maendeleo ya miundombinu. Katika kipindi cha uongozi wa bodi hiyo, pia iliwezesha ongezeko kubwa la wanachuo na wahitimu, ambapo jumla ya wanachuo 43,753 walihitimu katika kipindi cha miaka minne, huku wahitimu 37,792 wakitoka kwenye programu mbalimbali za mafunzo ya muda mrefu.
Dkt. Turuka ametaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kuimarishwa kwa tafiti na machapisho ya kitaaluma, ambapo jumla ya tafiti tumizi nane na machapisho 43 ziliandaliwa na chuo wakati wa kipindi hicho. Pia, bodi ilisimamia kwa karibu shughuli za mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi wa umma, ambapo zaidi ya watumishi 46,000 walihudhuria mafunzo mbalimbali, huku watumishi 4,149 wakifaulu mitihani ya utumishi wa umma. Pia Dkt. Turuka ametoa shukrani za dhati kwa mamlaka ya uteuzi, Menejimenti ya chuo, na wadau mbalimbali kwa usaidizi wao mkubwa wakati wa kipindi hicho cha uongozi. Akiwa ameteuliwa kwa kipindi cha pili, amewahakikishia wajumbe wa bodi mpya kuwa wataendeleza juhudi za kuimarisha chuo hadi kufikia malengo makubwa zaidi kwa maendeleo ya taifa
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo na Afisa Mtendaji Mkuu, Dkt Ern ambaye pia ni Katibu wa Bodi, akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya chuo kwa kipindi cha miaka minne amesema kuwa, katika kipindi hicho, chuo kimefanikisha kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma takribani 47,000, mara zaidi ya idadi iliyopatikana wakati wa bodi iliyopita. Mafunzo haya yamegawanyika katika makundi matano, ikiwa ni pamoja na mafunzo elekezi, mafunzo ya kuwajengea uwezo, mafunzo ya kujenga umahiri, mafunzo ya maadili na utawala bora, na mafunzo ya uongozi.
Aidha, Dkt. Mabonesho ameeleza kuwa chuo kimefanikiwa kufanya tafiti tumizi nane zenye lengo la kutatua changamoto za kiutendaji serikalini, huku pia ikichapisha machapisho 43 ya kitaaluma na kushiriki kwenye shauri za kitaalam 27 zinazolenga kuboresha mifumo ya utawala na usimamizi wa rasilimali watu. Amesema kuwa, awamu ya pili ya ujenzi wa Kampasi ya Singida imekamilika kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 2.2, huku ujenzi wa Kampasi ya Tanga ukiwa ukiendelea kwa kasi kwa ufadhili wa serikali.
Kuhusu usimamizi wa rasilimali watu, Dkt. Mabonesho alieleza kuwa hadi Septemba 2025, chuo kina jumla ya watumishi 372, kati yao 320 ni wa kudumu na wanaostahili malipo ya uzeeni. Kati yao, 176 ni wa kada ya kitaaluma na 144 wa kada za kiutawala. Chuo kinaendelea na mikakati ya kuendeleza watumishi kwa kutoa ruhusa kwa zaidi ya 30 kujiendeleza na kuajiri watumishi wapya, huku pia ikiondoa waliostaafu au kuhamia taasisi nyingine.
Bodi ilizinduliwa ina jumla ya wajumbe saba ikijumuisha Dkt. Florens Martin Turuka (Mwenyekiti), Dkt. Ernest Francis Mabonesho (Katibu), pamoja na wajumbe wengine: Mhe. Jaji (Mstaafu) Awadh Mohamed Bawazir, Prof. Masoud Hadi Muruke, Balozi John Ulanga, Dkt. Faraja Teddy Igira, na Bi. Leila Maurilyo Mavika.
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (katikati), akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri, Dkt. Florens Turuka, na kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo na Afisa Mtendaji Mkuu, Dkt. Ernest Mabonesho.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri (hawapo pichani) pamoja na Menejimenti na Wafanyakazi wa Chuo hicho, katika hafla ya Uzinduzi wa Bodi hiyo uliofanyika katika Kituo cha Mafunzo kwa njia ya mtandao cha Chuo cha Utumishi wa Umma jijini Dar es salaam.
Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Ernest Mabonesho akiwasilisha Taarifa ya Utendaji ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi (hayupo pichani) kuzungumza na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania pamoja na Menejimenti na Wafanyakazi wa chuo katika hafla ya uzinduzi wa bodi hiyo uliofanyika , jijini Dar es Salaam.
Wajumbe wa Bodi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Menejimenti na Wafanyakazi wa chuo hicho wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais- UTUMISHI (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao katika hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo jijini Dae es Salaam.
Menejimenti na Wafanyakazi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao katika hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo jijini Dae es Salaam.