
Dar es Salaam - Julai 28, 2025,
Mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wapya 105 wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), yanayofanyika kwa siku tano yamefunguliwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura A. Katunzi. Mafunzo haya yanatolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) katika ukumbi wa Maktaba, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Akifungua mafunzo, Dkt. Katunzi amesema kuwa kati ya waombaji 5,000 waliotuma maombi ya ajira, ni waombaji 105 pekee ndio waliofanikiwa kupata nafasi, sawa na asilimia 2%, hivyo amewapongeza watumishi wapya kwa fursa waliyopata, na kuwaeleza kuwa ajira zao zimetokana na mahitaji ya shirika ya kuimarisha ufanisi na utoaji wa huduma bora. Amesisitiza kuwa, kuajiriwa kwao kunatarajiwa kuleta ufanisi mkubwa katika shirika, hivyo kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha shughuli na malengo ya shirika.
Akiongea na washiriki, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Ernest Mabonesho, amesema kuwa utekelezaji wa Mafunzo Elekezi ni takwa la kisheria, kulingana na waraka wa utumishi No. 5 wa mwaka 2011, unaowataka waajiri kuwapatia waajiriwa wapya mafunzo ya awali. Amepongeza utekelezaji wa waraka huo na Mkurugenzi wa TBS kwa kuutekeleza kikamilifu.
Pia, Dkt. Mabonesho amewaambia washiriki kuhakikisha wanazingatia mafunzo haya, yenye lengo la kuwawezesha waajiriwa wapya kuelewa vyema utumishi wa umma na misingi yake, ikiwemo sheria, kanuni, na taratibu mbalimbali zinazotumika katika utendaji kazi serikalini.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura A. Katunzi akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mafunzo elekezi kwa Watumishi wapya 105 wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), katika ukumbi wa Maktaba, chuo kikuu cha Dar es Salaam jijini Dar es Salaam, tarehe leo Julai 28, 2025.
Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Ernest Mabonesho akiongea na Watumishi wapya 105 wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), katika ukumbi wa Maktaba, chuo kikuu cha Dar es Salaam jijini Dar es Salaam, tarehe leo Julai 28, 2025.
Picha ya baadhi ya watumishi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), wakati wa kufunguzi Mafunzo elekezi kwa Watumishi wapya 105 wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), katika ukumbi wa Maktaba, chuo kikuu cha Dar es Salaam jijini Dar es Salaam, Julai 28, 2025.