
Dar es Salaam, Septemba 1, 2025
Wajiriwa wapya 64 wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) wametakiwa kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia maadili ya kazi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo Elekezi ya awali kwa washiriki hao, Mkurugenzi wa Kampasi ya Singida, Dkt. Emmanuel Tandika ayemwakilisha Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu, ameeleza kuwa watumishi wa Umma wanapaswa kujua na kufanya kazi kwa kufuata sheria, kanuni, sera, na miongozo mbalimbali inayosimamia utumishi wa umma. Amesisitiza kuwa, mafunzo haya ni muhimu sana kwa watumishi ili kuwasaidia kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi zaidi.
Pia, Dkt. Tandika ameeleza kuwa, katika mafunzo hayo, washiriki watajifunza kuhusu Maadili ya Utumishi wa Umma, Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma, Misingi ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Mawasiliano ya Kiofisi, Muundo wa serikali na shughuli zake, pamoja na Utoaji wa huduma bora .
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa OSHA , Bw. Raphael Makoninde amewaeleza washiriki kuwa, mafunzo elekezi ni ya kisheria kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma na Walaka wa Utumishi Na. 5 ya mwaka 2011, ambao unawataka waajiri kuhakikisha kuwa watumishi wapya wanapatiwa mafunzo Elekezi ( Induction course) ndani ya miezi sita tangu kuajiriwa kwao. Hivyo amewaeleza washiriki kuzingatia mafunzo hayo ili kuelewa vyema sheria, kanuni, taratibu, na maadili yanayohusu utumishi wa umma.
Aidha, alibainisha kuwa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania ndicho chenye mamlaka ya kuendesha mafunzo haya.
Mafunzo haya yanaendeshwa kwa siku tano na Chuo cha Utumishi wa Umma- Kampasi ya Singida kuanzia leo, tarehe 1 hadi 5 Septemba 2025, katika Ukumbi wa OSHA, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma - Kampasi ya Singida, Dkt. Emmanuel Tandika, akizungumza na washiriki wakati wa ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa waajiriwa wapya wa Wakala wa Usalama na Afya mahali pa kazi yanayofanyika katika Ukumbi wa OSHA, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa OSHA, Bw. Raphael T. Makoninde akiongea na washiriki wa Mafunzo Elekezi kwa waajiriwa wapya wa Wakala wa Usalama na Afya mahali pa kazi yanayofanyika katika Ukumbi wa OSHA, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya waajiriwa wapya wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) wakisikiliza kwa makini wakati wa ufunguzi wa Mafunzo katika Ukumbi wa OSHA, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.