
Mafunzo ya siku nne ya kuwajengea uwezo watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) ngazi ya wilaya na makao makuu kuhusu Mwongozo wa Uendeshaji wa Mashauri ya Nidhamu na Rufaa kwa Walimu yamefunguliwa rasmi leo tarehe 5 Mei 2025. Mafunzo hayo, yanayofanyika katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Sehemu ya Mafunzo kwa njia ya Mtandao jijini Dar es Salaam, yanalenga kuboresha kwa kiasi kikubwa usimamizi wa utumishi wa walimu nchini na kuhakikisha utendaji wa haki na uwazi katika michakato ya nidhamu.
Akifungua mafunzo hayo, Mgeni Rasmi na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Prof. Masoud H. Muruke, alisisitiza umuhimu wa mafunzo hayo kama hatua muhimu katika kuimarisha uwajibikaji na maadili katika utumishi wa walimu. Prof. Muruke alitoa shukrani za dhati kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake na juhudi za kuimarisha taasisi zinazosimamia utumishi wa umma, ikiwa ni pamoja na Tume ya Utumishi wa Walimu.
Prof. Muruke alieleza kuwa lengo kuu la mafunzo haya ni kuwawezesha watumishi wa Tume kuwa na uelewa wa kina kuhusu Mwongozo mpya wa Uendeshaji wa Mashauri ya Nidhamu na Rufaa kwa Walimu. "Mafunzo haya yatawajengea uelewa wa kutosha washiriki kuhusu Muundo na Majukumu ya Tume na Kamati za Wilaya, pamoja na taratibu za ushughulikiaji wa mashauri ya nidhamu na rufaa." Amesema Prof. Mruke”
Alieleza matarajio yake kuwa mafunzo haya yatawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia kikamilifu sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo, hatimaye kutenda haki kwa walimu kwa kujituma na uaminifu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Ernest Mabonesho, alimshukuru Mwenyekiti na Katibu wa Tume kwa kuona umuhimu wa kuwajengea uwezo watumishi ili kuboresha utendaji wao wa kazi. Mgeni Rasmi kwa heshima ya kukubali mwaliko na kufungua mafunzo hayo. Alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa TPSC mwaka 2000, chuo hicho kimejitolea kuwajengea uwezo watumishi wa umma kote nchini kupitia matawi yake mbalimbali. Aidha, alibainisha kuwa mafunzo haya yameandaliwa mahsusi kwa Maafisa wa Tume ngazi ya wilaya na watumishi wengine ili kuwawezesha kusimamia mashauri ya nidhamu na rufaa za walimu kwa ufanisi, kwa kuzingatia sheria na taratibu husika. alieleza matarajio yake, akiitaja,
"Tunatarajia kuwa mafunzo haya yataongeza uadilifu, usawa na uwajibikaji, kupunguza ucheleweshaji wa haki, kukuza maadili kazini, na hatimaye kuimarisha tija katika utumishi wa walimu na utumishi wa umma kwa ujumla."Amesema Dkt. Mabonesho
Naye Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Mwl. Paulina M. Nkwama, alitoa shukrani kwa Mgeni Rasmi na washiriki wote 118. Alieleza kuwa mafunzo ni sehemu ya Programu ya Uboreshaji wa Kada ya Ualimu (TSP) inayofadhiliwa na GPE, ambapo Tume inatekeleza afua za motisha na uwajibikaji. Mwl. Nkwama alibainisha mafunzo yanatokana na Mwongozo mpya wa Uendeshaji wa Mashauri ya Nidhamu, uliotokana na changamoto za ukiukwaji wa sheria zilizosababisha mashauri kurejeshwa. Alisisitiza kuwa mafunzo yataongeza uelewa wa sheria na taratibu za mashauri, hatimaye kuhakikisha haki, uwazi, ufanisi na kuepusha ucheleweshaji.
Mafunzo hayo yanayowezeshwa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, yanayojumuisha washiriki kutoka wilaya za mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Morogoro, Mbeya, Songwe, pamoja na maafisa wa makao makuu ya Tume, na yanatarajiwa kumalizika tarehe 8 Mei 2025.
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Masoud H. Muruke, akifungua Mafunzo kwa watumishi wa Tume wa ngazi za wilaya na makao makuu kuhusu Mwongozo wa Uendeshaji wa Mashauri ya Nidhamu na Rufaa yaliyofanyika katika Chuo cha Utumishi wa Umma, Dar es Salaam tarehe 5 Mei, 2025.
Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Dkt. Ernest Mabonesho akizungumza na washiriki wakati wa ufunguzi wa Mafunzo kwa watumishi wa Tume wa ngazi za wilaya na makao makuu kuhusu Mwongozo wa Uendeshaji wa Mashauri ya Nidhamu na Rufaa yaliyofanyika katika Chuo cha Utumishi wa Umma, Dar es Salaam tarehe 5 Mei, 2025.
Katibu wa Tumeme ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama akitoa neno la utangulizi wakati wa ufunguzi wa Mafunzo kwa watumishi wa Tume wa ngazi za wilaya na makao makuu kuhusu Mwongozo wa Uendeshaji wa Mashauri ya Nidhamu na Rufaa yaliyofanyika katika Chuo cha Utumishi wa Umma, Dar es Salaam tarehe 5 Mei, 2025.
Picha ya pamoja ya baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya Uendeshaji wa Mashauri ya Nidhamu na Rufaa kwa Walimu (ngazi ya wilaya na makao makuu) na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Masoud H. Muruke, baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo TPSC, Dar es Salaam, tarehe 5 Mei, 2025. Wengine walio katika picha ni Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa TPSC, Dkt. Ernest Mabonesho (kushoto kwa Mwenyekiti), na Katibu wa Tume, Mwl. Paulina Nkwama (kulia kwa Mwenyekiti).
Picha ya pamoja ya baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya Uendeshaji wa Mashauri ya Nidhamu na Rufaa kwa Walimu (ngazi ya wilaya na makao makuu) na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Masoud H. Muruke, baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo TPSC, Dar es Salaam, tarehe 5 Mei, 2025. Wengine walio katika picha ni Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa TPSC, Dkt. Ernest Mabonesho (kushoto kwa Mwenyekiti), na Katibu wa Tume, Mwl. Paulina Nkwama (kulia kwa Mwenyekiti).