Imewekwa: 31 May, 2025
WAZIRI SIMBACHAWENE: SERIKALI INA MATARAJIO MAKUBWA KWA CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA KATIKA KUJENGA UWEZO WA WATUMISHI WA UMMA NCHINI.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ina matarajio makubwa na Chuo kwa kuwajengea uwezo watumishi wa Umma na kutoa wahitimu mahiri na wenye uzalendo wanaoleta chachu ya maendeleo nchini.

Mhe. Simbachawene amesema hayo leo tarehe 30 Mei, 2025 kwenye Mahafali ya 41 ya kuwatunuku wahitimu wa ngazi mbalimbali wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika katika Ukumbi wa Social Rwoma RC Mission mkoani Singida.

Mhe. Simbachawene amesema kuwa chuo cha utumishi wa Umma ni sehemu muhimu ya serikali katika kujenga nguvu kazi yenye weledi wa hali ya juu, na serikali ina matarajio makubwa kuhusu utekelezaji wa mipango ya kuimarisha uwezo na umahiri wa watumishi wa umma kupitia chuo cha Utumishi wa Umma.

“Serikali ina matarajio makubwa na Chuo cha Utumishi wa Umma   katika utekelezaji wa mipango ya serikali ya kujenga uwezo na umahiri wa watumishi wa umma” Mhe. Simbachawene alisisitiza

Mhe. Simbachawene amewataka wahitimu walioajiriwa katika Utumishi wa Umma na watakaoajiriwa kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma ikiwa ni pamoja na kutunza siri za Serikali na kuepuka rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao na wahitimu ambao hawana ajira kutumia ujuzi walioupata kujiajiri kwa maendeleo ya taifa.

 

Aidha, Mhe. Simbachawene, amewapongeza wahitimu wote waliomaliza ngazi mbalimbali na kuwahimiza kutumia taaluma zao kwa manufaa ya taifa, kwa kuondoa rushwa, kutekeleza maadili mema, na kujikinga na magonjwa hatari kama ukimwi.

Vile vile, Waziri Simbachawene, amepongeza menejimenti chuo kwa  mafanikio ya chuo katika kuboresha miundombinu kwa kujenga kampasi ya Singida kwa kutumia fedha za ndani, na kueleza kuwa serikali itaendelea kutoa ruzuku ya maendeleo kwa chuo ili kuimarisha miundombinu na kukabiliana na changamoto za kifedha, ikiwemo ujenzi wa kampasi mpya na uboreshaji wa miundombinu iliyopo katika kampasi za Dar es Salaam na Tabora.

Kwa upande wa Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu, Dkt. Ernest Mabonesho, wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji wa chuo katika mahafali amesema kuwa jumla ya wahitimu ni 1,330 wametunukiwa Shahada ya kwanza, Stashahada na Astashahada ya Ufundi katika fani mbalimbali wametukiwa

Aidha, Dkt. Mabonesho amesema, Chuo kimeendelea kutekeleza majukumu yake msingi kwa kutoa mafunzo, kufanya tafiti, kutoa ushauri wa kitaalamu, na kusimamia miradi ya maendeleo. Kwa mwaka huu wa fedha wa 2024/2025, chuo kimedahili jumla ya wanafunzi 10,507 kwa mafunzo ya muda mrefu kutoka ngazi ya astashahada hadi shahada ya kwanza. Pia, jumla ya  watumishi wa umma 11,122 walipata mafunzo ya muda mfupi.

Katika kutekeleza miradi ya maendeleo, Dkt. Mabonesho amesema kuwa Chuo kinakamilisha hatua za mwisho za umaliziaji wa ujenzi wa majengo ya Chuo katika Kampasi ya Singida ambapo mpaka sasa ujenzi umekamilika kwa asilimia 99% na chuo kinategemea kuanza kutumia majengo hayo kwa mwaka wa masomo 2025/2026.

Aidha, Dkt. Mabonesho ameishukuru Chuo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kutenga fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 1.5 katika Bajeti ya mwaka 2024/25 na kiasi cha Shilingi Bilioni 2.6 katika bajeti ya Mwaka 2025/2026 ujenzi wa majengo ya chuo ya Kampasi ya Tanga ambao umeishaanza.

Pia, Dkt. Mabonesho amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza vyema Serikali ya Awamu ya Sita, pamoja na Mhe. Simbachawene kwa utendaji bora katika kutekeleza majukumu ya ofisi yake.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma SACP Ibrahim Mahumi aliyemwakilisha     amesema, Chuo cha Utumishi wa Umma kina dhima kubwa ya kuandaa watumishi wa umma na kazi hiyo imekuwa ikifanywa na chuo kwa kutoa wahitimu ambao ni muhimu kwa utendaji kazi katika utumishi wa umma.

 Awali akitoa salamu za Bodi ya Ushauri ya chuo, mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ambaye ni mjumbe wa Bodi Prof. Masoud Muruke amesema, Chuo cha Utumishi wa Umma kimeendelea kuwa chachu ya maendeleo ndani ya taifa letu kwa kutoa mafunzo wezeshi kwa wananchi na watumishi wa taasisi mbalimbali, Shauri za Kitaalamu na kufanya Tafiti Tumizi zinazolenga kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili Utumishi wa Umma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na wahitimu wa kozi mbalimbali (hawapo pichani) katika mahafali ya 41 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika katika Ukumbi wa Social RC Mission Singida, Manispaa ya Singida.

Sehemu ya Wahitimu wa Astashahada, Stashahada na Shahada ya kozi mbalimbali wakimsikiliza mgeni rasmi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) wakati wa mahafali ya 41 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika katika Ukumbi wa Social RC Mission Singida, Manispaa ya Singida.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (mwenye kofia nyekundu) akiteta jambo na Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Prof. Masoud Muruke (wa kwanza kulia) ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa bodi hiyo kwenye Mahafali ya 41 wakati Waziri huyo alipowatunuku wahitimu wa ngazi mbalimbali wa chuo hicho (hawapo pichani) yaliyofanyika katika Ukumbi wa Social Rwoma RC Mission mkoani Singida. Wa kwanza kushoto ni Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Ernest Mabonesho.

Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Ernest Mabonesho akiwasilisha taarifa ya utendaji wa chuo kwa mgeni rasmi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene wakati wa mahafali ya 41 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika katika Ukumbi wa Social Rwoma RC Mission mkoani Singida.

Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo